Home Top Ad

Responsive Ads Here

Polisi yaanza kuwasaka walioua askari 4, Mbagala

Watu 13 wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamewaua polisi wanne katika uvamizi wa Benki ya CRDB eneo la Mbande kata ya Mbagala wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, na kutoweka na kusikojulikana.




Akizungumza na East Africa radio, leo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa limetokea jana majira ya saa moja na nusu jioni wakati askari hao wakibadilishana lindo na ndipo walivamiwa na majambazi hao.
Kamanda Sirro amesema kuwa licha ya kufanya tukio hilo pia majambazi hao walivamia kituo cha polisi cha Mbande na kisha kuchukua sare ya polisi na kukimbia nazo ambapo amesema jeshi la polisi linaendelea kuwasaka wahusika wa tukio hilo.
Aidha Kamanda huyo wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ametumia Fursa huyo kuwataka Wakazi wa Dar es Salaam kuwa watulivu na kushirikiana na jeshi hilo kutoa taarifa kufanikisha kuwakamata watu hao ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo limetaja majina ya askari waliopoteza maisha katika tukio hilo.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Polisi, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Nsato Marijani Mssanzya amesema katika tukio hilo majambazi hayo yalipora silaha mbili aina ya SMG pamoja na risasi sitini, hakuna fedha wala mali ya benki ya CRDB iliyoibiwa ama kuharibiwa.
CP Mssazya amewataja askari polisi waliofariki katika tukio hilo kuwa ni askari namba E.5761 CPL Yahaya, F. 4660 CPL Hatibu, G.9524 Tito pamoja na G. 9996 PC Gastone, pia na raia waliojeruhiwa ni Ally Chiponda na Azizi Yahaya wote wakazi wa Mbande.
Katika hatua nyingine, Kamishna Nsato amekemea wanasiasa wanaoendelea kufanya mikutano ya siasa ambayo tayari jeshi hilo limeipiga marufuku isifanyike sehemu yeyote nchini na tayari linawashikilia baadhi ya watu kwa mahojiano zaidi.
Amesisitiza kuwa kuanzia sasa hata mikutano ya ndani ya vyama vya siasa haitaruhusiwa kwa madai kuwa baadhi ya mikutano au vikao hivyo hutumika kupanga njama za kuvunja amani ya nchi.
Amewatoa hofu wananchi pindi waonapo jeshi hilo la Polisi linafanya mazoezi sehemu mbalimbali kwani vitendo hivyo ni njia mojawapo ya kuhakikisha usalama wa nchi unazingatiwa na kila mwananachi anakua salama katika eneo lake.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba aliyefika eneo la tukio usiku huo huo amesema askari hao walivamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha katika eneo hilo na kuwaua askari hao waliokuwa wakishuka kwenye gari tayari kwa kupokezana lindo.
Amesema mbali na vifo hivyo, pia raia wawili wamejeruhiwa na wanaendelea na matibabu.
Waziri Nchemba amesema mbali na kulaani tukio hilo amewataka wahusika kujisalimisha na wananchi kutoa ushirikiano.
“Hatutaishia kulaani tu tukio hili na matukio mengine kama haya,natoa rai kwa wahusika kujisalimisha.Vilevile wananchi na raia wema tunaomba ushirikiano wenu katika vita hii ya kupambana na wahalifu hawa na wanaotuzunguka kwenye maeneo yetu”. Amesema Waziri Mwigulu
Polisi yaanza kuwasaka walioua askari 4, Mbagala Polisi yaanza kuwasaka walioua askari 4, Mbagala Reviewed by pongwa trading on 11:11:00 Rating: 5

No comments

Recent