Mbeya City waitawanya SIMBA
Vinara wa ligi kuu Tanzania Simba SC ambao wapo kwenye mbio za ubingwa msimu huu, wamekwaa kisiki hii leo katika dimba la taifa baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Mbeya City kutoka Jijini Mbeya na hivyo kugawana pointi moja kila timu.
Katika mchezo huo uliokuwa wa wazi na wenye kila aina ya burudani za soka, Mbeya City ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 37 kupitia kwa Ditram Nchimbi baada ya mabeki wa Simba kupotena, kabla ya Simba kusawazisha katika dakika ya 66 kufuatia mpira wa adhabu ndogo iliyopigwa na Ibrahim Ajibu nje kidogo ya box na kuingia wavuni moja kwa moja.
Kocha wa Mbeya City alifanya mabadiliko ya kumtoa Mrisho Ngassa na kuingia Ayoub Semtawa ambaye alitumia vizuri 'gap' ambalo lilikuwa likiachwa na beki wa Simba Mohamed Hussein aliyekuwa akipanda mbele mara kwa mara na kutoa kros safi iliyomaliziwa kiufundi na nahodha wa Mbeya City Kenny Ally dakika ya 79 na kuandika bao la pili.
Simba ilimtoa Ajibu na kumuingiza Mohamed Ibrahim, huku ikicharuka zaidi kwa kosa kosa za hapa na pale, na kufanikiwa kupata penati baada ya Mohamed Hussein kuangushwa katika eneo la hatari, penati iliyofungwa na Shiza Kichuya katika dakika ya 86.
Simba iliendelea kutengeza nafasi nyingi lakini mshambuliaji wake Laudit Mavugo alishindwa kuzitumia ipasavyo na hadi mwisho wa mchezo, Simba 2, Mbeya City 2.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha point 55 ikiwa mbele kwa point tatu dhidi ya Yanga ambao kesho wanakipiga na Mtibwa Sugar katika dimba la Jamhuri Morogoro.
Katika michezo mingine iliyopigwa leo, Kagera Sugar imeifunga Majimaji bao 1-0 mjini Bukoba kwa bao la Mbaraka Yusuph ambaye sasa amefikisha mabao 10, huku Toto Africans wakilipiza kisasi kwa Mbao FC kwa kuichapa mabao 2-0 katika dimba la CCM Kirumba.
Mbeya City waitawanya SIMBA
Reviewed by Unknown
on
05:51:00
Rating:
No comments