Home Top Ad

Responsive Ads Here

MAJIBU YA CUF

MAJIBU YA CUF KWA IBRAHIMU LIPUMBA KUTOKANA NA MAHOJIANO ALIYOFANYA LEO KATIKA KIPINDI CHA FUNGUKA KILICHORUSHWA NA AZAM TV (TWO) AKIHOJIWA NA MKURUGENZI WA KITUO HICHO NDUGU TIDO MUHANDO:

The Civic United front (CUF-Chama Cha Wananchi) kama ilivyowajulisha hapo awali kuwa itatoa taarifa sahihi za Taasisi kwa lengo la kuweka sawa na kuujulisha umma pale patakapotokea upotoshwaji wa masuala mbalimbali yanayohusiana na Chama chetu cha CUF kwa kukusanya taarifa za wiki zima zilizochanya (positive) na au zile hasi (negative) dhidi ya Chama kwa lengo la kuupotosha umma ili wanaChama, viongozi wa Chama, na wananchi kwa ujumla waweze kuwa (updates) na kukaa katika mstari uliosawa kitaarifa. (Weekly CUF information/news review). Leo tarehe 5/2/2017 muda wa saa 3 mpaka saa 4 asubuhi kituo cha luninga cha Azam TV Two kupitia kipindi cha FUNGUKA warusha hewani mahojiano yaliyofanywa kati ya Mkurugenzi wa kituo hicho Ndugu Tido Muhando na Ibrahim Lipumba. Awali napenda kuchukua fursa hii kumpongeza muongozaji wa kipindi hicho ndugu Tido Mhando, mwandishi wa habari nguli wa muda mrefu katika tasnia hii kwa umahiri wake katika uendeshaji wa kipindi pamoja na kuwa na maswali chokonozi (critical questions). Kipindi amekiendesha vyema na kimeweza kumfanya muulizwaji kujibu maswali hayo kwa kujikanganya sana.

Katika mahojiano hayo hakukuwa na jambo jipya lolote kutoka kwa muhojiwa zaidi ya yale yale tuliyowahi kuyasikia kutoka kwake na hasa kwa wale wanaofuatilia masuala ya siasa isipokuwa mambo mawili; Moja Ibrahimu Lipumba ameonyesha kutokujua jinsi ya muundo wa Muungano wa Mkataba unavyokuwa na suala la pili ni kwa mara ya kwanza tangu wizi wa fedha za Ruzuku kufanyika tarehe 5 January, 2017 leo amejitokeza hadhara na kujaribu kueleza jinsi walivyofanya wizi huo wa kuchepusha shilingi 369 milioni kinyume na katiba na taratibu za Chama. Masuala hayo na mengine yatafafanuliwa katika taarifa hii kwa mukhtasari. Tulichojifunza ni kwamba Ibrahimu Lipumba amepoteza uwezo na nguvu ya kujenga hoja, lakini pia amepoteza muelekeo wa kisiasa na kumsababisha kujitia msongo wa mawazo ambao kama angekubaliana na ushauri aliopatiwa hapo awali asingeweza kufika hapa alipojifikisha. Amepoteza heshima aliyojijengea kwa watanzania, wanaCUF na watanzania wengi wapenda mabadiliko nchini. Aidha yapo machache ambayo ameyaeleza vizuri na kwa usahihi.

Kwa mukhtasari tunapenda kufanya majumuisho na kujibu hoja alizozitoa kwa upotoshwaji na au kutokujua kama ifuatavyo:

1. Kuhusu Muungano wa Mkataba;
Lipumba ameeleza kuwa afahamu nini maana ya Muungano wa Mkataba na muundo wake jinsi ulivyo? Na kwamba alitofautiana na Chama kuhusu suala hilo. Hili si suala geni limeelezwa kwa kirefu sana na wasomi waliobobea katika fani ya sheria na kufanyiwa uchambuzi na waandishi kadhaa wa habari kwa kuandikia makala za kuelezea dhana sahihi ya Muungano wa Mkataba. Ni ukweli kuwa CUF kwa wakati uliopita ulikuwa unaamini juu ya sera ya muundo wa Muungano wa serikali tatu. Lakini sera ni muongozo tu wa jinsi ya suala husika makhsusi namna linavyotakiwa kushughulikiwa. Sera inaweza kubadilika kulingana na haja, wakati, na malengo husika yanayokusudiwa kufikiwa kwa dhamira njema. Wazanzibari kwa ujumla wao bila ya kujali itikadi ya vyama ukiondoa wahafidhina wachache wanaonufaika na mfumo uliopo sasa, wanadai mamlaka kamili ya nchi yao. Mamlaka kamili ya nchi yao yatapatika kwa kuwa na Muungano ulioundwa katika mfumo sahihi. Treat based union (Muungano wa mkataba) ni njia sahihi ya kulinda mamlaka kamili ya nchi ya Zanzibar. Jaji Mstaafu wa mahakama kuu Mheshimiwa Abubakari Khamisi aliwahi kuwasilisha mada kamili chini ya uenyekiti wa Ibrahimu Lipumba wakati huo pale katika ukumbi wa PTA Sabasaba, Dar es Salaam tarehe 23 Disemba mwaka 2013. Hakuna mzanzibar anayekataa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.  Inasikitisha lakini haishangazi sana kwa kuwa Lipumba ni msomi wa fani ya uchumi na si sheria. Hata hivyo kama una nia njema kwa kupitia maandiko ya jambo husika kwa usomi wa mtu alionao hata kwa fani tofauti umfanya muhusika kuwa na uelewa wa haraka ya nini kinachokusudiwa na ukapata mantiki ya hoja zinazoelezwa.
Muungano wa kikatiba kama huu uliopo sasa wa mwaka 1964 ulioasisiwa na msingi wa Mkataba wa Muungano (Articles of Union) una athari kubwa kwa pande zote mbili na hasa kwa Zanzibar kwa udogo wake na kwa kupoteza mamlaka yake ya asili. Unapozungumzia Muungano wa mkataba (Treat based Union) unakusudia mahusiano yatakayojengwa kwa kuirejeshea Tanganyika na pia Zanzibar mamlaka yao kamili ya kidola na yatawezesha kuwapo na utaratibu wa ushirikiano kati ya nchi mbili zilizo sawa na zilizo huru na zenye mamlaka kamili ya kidola. Mkataba utaoongoza mahusiano hayo utaweka wazi A-Z ni mambo gani nchi hizo zitashirikiana na namna ushirikiano wao utavyopaswa kuwa. Pale nchi iliyo na mamlaka yake kamili inapoandikiana mkataba wa kuwa na ushirikiano au muungano na nchi nyingine inakuwa haiyapotezi mamlaka yake au uhuru wake.  Hali hiyo ni kinyume na Muungano wa kikatiba uliopo sasa ambao umeifanya Zanzibar iyahaulishe kwenye Serikali ya Muungano mamlaka na madaraka yake ya kimsingi. Zanzibar imezitoa mhanga nguvu zake za kidola wakati mwenzake Tanganyika haikulazimika kujitosa na kutoa mhanga kama huo kwa vile utawala wa Tanganyika unaendeshwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Tunamtaka Lipumba na wenzake wanaofanana kifikia wafahamu kuwa ushirikiano au muungano wa Mkataba ni kwamba kila nchi iliyotia saini mkataba wa muungano inakuwa na nguvu ya ‘turufu’.  Hivyo hata katika mambo yaliyokubaliwa kuingizwa katika ushirikiano nchi inayohusika inaweza kuitumia nguvu yake ya turufu na ikaomba hifadhi ya watu wake endapo inahisi kwamba inahatarishwa na sera za huo muungano katika utekelezaji wa mahusiano na ushirikiano wa nchi hizo. Muungano wa aina hiyo, yaani wa Mkataba, utairejeshea Serikali ya Umoja wa Kitaifa mamlaka na  madaraka muhimu ambayo Zanzibar haikuwa nayo kwa muda wa miaka 52 sasa.  Yakitumiwa vyema madaraka hayo yataiwezesha Zanzibar kutekeleza sera zitazoirejeshea Zanzibar adhama na fahari iliyokuwa nayo zamani na kuifanya ishiriki kikamilifu katika shughuli za kanda ya Afrika ya Mashariki na ya Kati na kupindukia mipaka ya kanda hii.
Athari za Muuungano wa Kikatiba tuliona hivi sasa:
• Miaka 50 ya Muungano haikuinufaisha Zanzibar inavyostahiki kiuchumi, kisiasa, kiusalama, na kijamii.
• Muungano umeifanya Zanzibar itoweke kwenye ramani ya dunia.
• Muungano umeifanya Zanzibar idhurike kisiasa, kiuchumi na kijamii ikilinganishwa na visiwa vingine kama vile Mauritius na Seychelles.
• Muungano umesababisha dhiki za kiuchumi na shida za kijamii zinazoisibu Zanzibar kwa muda wa takriban nusu karne.
• Muungano umewadhalilisha na kuwaondolea amani na utulivu wa kisiasa wazanzibari na kusababisha maafa makubwa hasa kila unapofanyika uchaguzi ambao usimamiwa na vyombo vya dola vya Muungano/Tanganyika.
• Muungano umeiondolea Zanzabar Hadhi na heshima yake kitaifa na kimataifa.
• Muungano umeifanya Zanzibar kushindwa kujiamulia njia ya kiuchumi na kijamii ya kuifuata ili iweze kujikomboa kutokana na mateso, shida na dhiki ilizo nazo.
• Muda wa miaka 50 serikali ya Muungano haikuyatumia vyema madaraka iliyoyatwaa kutoka Zanzibar kupigana na adui ujinga, maradhi, ubadhilifu, matumizi mabaya ya madaraka na umasikini.
• Muungano wa Mkataba kikatiba hautoi fursa/nafasi kwa njia nafuu ya kuufanyia marekebisho kila inapobidi kufanya hivyo ikilinganishwa na Muungano wa Mkataba.
Kwa mukhtasari huu ndio Muungano wa Mkataba. Na faida zake ni kinyume na athari tulizozieleza katika nukta 9 hapo juu. Lipumba anapaswa kufahamu kuwa kwa vyovyote iwavyo mapambano ya wazanzibari na watanganyika madhubuti walio makini katika kudai haki na usawa katika Muungano wetu hayatarejeshwa nyuma.

2. Kuhusu UMOJA WA KATIBA YA WANANCHI-UKAWA;
KWA bahati njema sana katiba ya CUF haitoi nafasi kwa masuala makubwa kuamuliwa na mtu au kiongozi mmoja kama zilivyo katiba ya vyama vingine. Mathani vyama vingine Katibu Mkuu wa Chama anateuliwa na Mwenyekiti wa Chama pekee. Ndani ya CUF hilo na mfano wa hayo halipo. Lazima masuala yapitie ndani ya vikao vya maamuzi na vina mamlaka ya kukubali au kukataa pendekezo lolote litakalowasilishwa katika kikao husika na kiongozi yeyote yule aliyepewa mamlaka ya uteuzi. Suala la mashirikiano ya vyama si jambo geni nchini iwe katika msuala ya ajenda mahususi au wakati wa uchaguzi. Mwaka 2000 CHADEMA haikusimamisha mgombea urais, chini ya uenyekiti wa Mzee Mtei na Katibu wake marehemu Bob Makani walimuunga mkono mgombea wa CUF wa urais(ambaye alikuwa yeye Lipumba). UKAWA uliasisiwa na Ibrahimu Lipumba na wenzake wakiwa katika bunge la katiba kule Dodoma. Maalim Seif Hakuwa mbunge wa bunge la katiba. Na baadae suala hilo likawasilishwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya Taifa, kisha Baraza KUU la uongozi Taifa, na baadae kuridhiwa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CUF uliofanyika Ubungo Plaza Juni 27-29 mwaka 2014. Suala la UKAWA si la mtu ni la maamuzi ya Chama. Lakini vikao hivyo pia vilijadiliana na kupitisha kuwa kutokana na kukwama kwa upatikanaji wa katiba, UKAWA kama mashirikiano ya vyama uende mbali zaidi ya katiba na bali uwaunganishe watanzania kuelekea uchaguzi wa seriakli za mitaa, vijiji na vitongoji na uchaguzi mkuu mwaka 2014/15. Yeye Lipumba anayepinga UKAWA mamlaka hayo ameyapata wapi nje ya vikao vya Chama ambavyo vilisharidhia uwepo wa UKAWA? Kikao gani cha Chama kimetengua maamuzi ya kuendeleza mashirikiano katika UKAWA? Uwepo wa changamoto za mashirikiano hauondoi uhalali wake na viongozi wote wa CUF wanatambua hilo.

CUF haijutii kumkaribisha Na kumuunga mkono Lowassa ndani ya UKAWA. Lipumba binafsi amehusika kwa namna moja au nyingine kumkaribisha Mheshimiwa Edward Lowassa kujiunga na UKAWA pamoja na kutoa wito kwa wanaChama wengine wa vyama mbalimbali, awaeleze watanzania wakati anafanya hayo na Video Clips zipo, alikumbwa na ‘pepo’ gani la kinyamwezi au kisukuma lililomfanya nafsi na dhamira kumsuta? Anamlaumu Katibu Mkuu kuzungumza na viongozi wenzake wa vyama kwani Lipumba hajui kuwa huo ni wajibu na kazi za Katibu Mkuu zilizoainishwa kikatiba Ibara ya 93 (1)(e)? Wakati akilaumu hivyo kikao gani cha Chama kilimruhusu kwenda kuzungumza na Dr.Wilbroad Silaa na George Kahangwa na wao kukubaliana kuwa Dr. Slaa awe mgombea wa UKAWA? Wapi katiba ya CUF inampa mamlaka ya yeye kufanya maamuzi hayo kwa niaba ya Chama? Yeye ni msemaji mkuu wa Chama kutokana na yale yaliyoazimiwa na kukubaliwa na vikao na si kujisemea lolote atakalo ambalo linapingana na Chama. Kama anamtuhumu Katibu Mkuu wake kwa wakati huo akifanya vikao bila yeye kuwa na taarifa aliwasilisha malalamiko hayo katika kikao gani cha Chama ili kuyashughulikia masuala hayo? Kwanini alianzisha mahusiano yasiyorasmi na baadhi ya viongozi wa ACT na kupokea fedha kutoka huko zikitoka kwa ‘system’ kufanya ziara na hata kujitangaza kuchukua fomu ndani ya Chama pale Ubungo plaza kwa gharama zisizotokana na Chama? Wala viongozi wenzake kujua kinachoendelea hali alikataa alipoulizwa ndani ya kikao cha baraza kuu la uongozi Taifa na Bi Fatma Kalembo kama anataka kugombea urais? Alijibu kuwa hana mpango huo itategemea maamuzi ya Chama.

Dr. Slaa aliyempendekeza kugombea urais mwaka 2015 amebadilika nini? Huyu si ndio yuleyule aliyesema kuwa alilazimika kunusuru Jahazi kwa maana ya kumsaidia Kikwete ashinde mwaka 2010? Dr. Slaa alikuwa fisadi wakati ule kuliko Kikwete? Maamuzi ya mashirikiano ya UKAWA yamefanywa na vikao halali na pia kumfanya Edward Lowassa kuwa mgombea wa UKAWA yalifanywa na vikao halali vya Chama. Si maamuzi ya Maalim Seif Sharif Hamad kama anavyotaka kuwapotosha watanzania. Hata hivyo Tunashukuru kwa kukiri kwake na kujibu vizuri swali la kuwa parcentage zake za kura zimekuwa zikishuka mwaka hadi mwaka na kwamba amepoteza mvuto kwa wananchi. Lakini pia swala la kumkaribisha Lowassa ilikuwa ni stratejia nzuri kwa upinzani kuweza kuishinda CCM na kwamba hauwezi kuongoza nchi kama hujakubalika na wananchi (wapiga kura), na yeye alikwenda nyumbani kwa Lowassa akiwa na mhe Mbatia na kufanya mazungumza nae ili awe mgombea wa UKAWA. Anachopaswa kufahamu Lipumba ni kwamba Chama cha CUF hakijawahi kupoteza Umoja wake katika kushughulikia masuala yeyote yale kupitia vikao halali vyake vya ndani ya Chama na hata alipoondoka kwa kujiuzuru CUF kama taasisi imara na viongozi makini walioongzwa na Jemedali Mkuu wa mapambano hayo Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad akishirikiana na wasaidizi wake waliweza kukivusha Chama katika uchaguzi mkuu Oktoba 25, 2015 na kupata mafanikio makubwa kisiasa kwa kushinda Uchaguzi wa Urais Zanzibar, wawakilishi na wabunge na madiwani wengi kwa pande zote mbili za Muungano. Na mgombea wa UKAWA alipewa na Tume ya taifa ya uchaguzi asilimia 39.8 ya kura na kampeni kuendeshwa kisasa kabisa. Kama mafanikio haya anadhani yamepatikana kupitia mganga wa kienyeji kutoka Nigeria kama anavyosema huko ni kupoteza uwezo wa uchambuzi wa kisayansi katika nyanja ya siasa.

3. Kuhusu kujiuzulu na kisha kutengua kujiuzulu kwake:
Lipumba alijiuzulu kwa hiyari yake bila kushurutishwa ambayo ni haki yake kikatiba. Ila tunashaangaa wajumbe gani hao kwa uwingi wao waliokuwa wanamfuata kumtaka arejee katika Chama? Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa kwa wingi wao ndio hao waliomfukuza uanaChama? Lakini ni wapi katika katika ya CUF inaruhusika kiongozi akijiuzulu anaweza kutengua maamuzi yake? Kifungu hicho cha katiba kiko ukurasa wa upi? Unawezaje kuhudhuria katika mkutano/kikao kisichokuhusu kwa njia ya kupigiwa simu na watu wasiofahamika na wala bila ya kualikwa rasmi na mamlaka husika? Mjumbe wa mkutano mkuu wa Chama ana mamlaka ya kumualika mtu katika mkutano? Pili kama alikuwa hakualikwa, na yeye anadai kuwa ndiye ‘Mwenyekiti halali’ wa CUF iweje CUF iandae mkutano mkuu ambao ulipaswa uendeshwe na ‘mwenyekiti halali’ ambaye  alikuwa anasubiri kualikwa? Mwenyekiti halali wa kikao anasubiri kualikwa katika kikao alichopaswa kukiongoza? Kwani lipumba ulifukuzwa au kusimamishwa uanaChama sasa unahitajika katika mkutano mkuu ujieleze kana kwamba kulikuwa na rufaa yako iliyopaswa kusikilizwa? Lipumba si amejiuzulu mwenyewe? Katiba ya CUF inamtaka kiongozi aliyejiuzulu aende mbele ya mkutano mkuu ajieleze kwanini amejiuzulu na aeleze sababu zake za kujiuzulu? Wapi yanapatikana hayo katika katiba ya CUF? Kwanini Lipumba avamie mkutano, kuharibu vifaa, kufanya fujo, akiongozwa na askari polisi? Kama sisi wenyewe tungeweza kuyaongea na kumaliza tofauti zilizojitokeza na kwamba haikupaswa suala hili kufikishwa mahakamani! kwanini Lipumba alikwenda kwa Msajili kutaka msaada ambao unaonekana ulikuwa unaratibiwa kwa nija ya kificho? na mara zote alikuwa anadai anasubiri maamuzi ya Msajili ili aanze kazi rasmi ya uenyekiti? Kwanini urejee ofisini kwa kukusanya wahuni na kupiga watu, walinzi na kuvunja milango ya ofisi? Katibu Mkuu gani atakayekuja kufanyakazi na wewe katika mazingira hayo? Lipumba hukusema kweli kuhusu saluti uliyopigiwa na askari pale buguruni wakati unazoa takataka, saluti ile sio ya diwani kama ulivyodai. Heshima hii inayopewa na viongozi wa CCm na kufikia kukiita Jembe inathibitisha jinsi unavyowatumikia vyema. Heshima hii unayopewa na jeshi la polisi, na kupewa ulinzi kila unapokwenda haihitajiki tochi kujua Lipumba wa mwaka 2010 siye wa mwaka 2017 na Jeshi la polisi linasimamia matukio ya kuuhalifu yanayofanywa na wafuasi wako bila ya kuchukua hatua zozote za kisheria. Uswahiba huu na serikali ya CCM na kila kukicha mguu na njia kuelekea Ikulu hakuna mpinzani wa kweli atakayekuamini tena kuongoza harakati za ukombozi na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini.

4. Kuhusu wizi wa Ruzuku ya Chama:
Lipumba amekiri kuwa wamefanya wizi huo kutokana na ukame na njaa iliyokuwa inawakabili. Lakini anakiri kuwa mamlaka ya fedha ni ya Katibu Mkuu isipokuwa akiwasiliana nae hajibu simu zake na kwamba hajafika ofisini. Lipumba anapaswa kufahamu kuwa suala hili si la Maalim Seif na Lipumba. Maamuzi ya vikao vya Chama yamefanyika kumfukuza uanaChama Lipumba na wenzake kutokana na mwenendo wao usiofaa unaokiuka taratibu, kanuni na katiba ya Chama. Hakuna uteuzi wowote utakaoufanya ambao utakubalika na Chama. Lakini hata kama Lipumba angelikuwa Mwenyekiti Halali wa CUF ili uteuzi uwe sahihi lazima uteuzi huo uthibitishwe yaani ukubaliwe na kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa kwa mujibu wa katiba ya Chama Ibara ya 91(f) jambo ambalo halijafanyika na halitafanyika kwa sababu Lipumba hana Kamati ya Utendaji ya Taifa wala hana ridhaa ya wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa wala hana bodi ya wadhamini inayomuunga mkono. Kilichofanyika ni wizi na hatua za kisheria kwa wahusika wote zishachukuliwa na Chama.

5. Kuhusu njia ya kuupatia ufumbuzi unaoitwa mgogoro ndani ya Chama:
Lipumba anasema tukae tulimalize suala hili kwa kuongea sisi wenyewe. Jambo hilo haliwezekani kwa kuwa kama kupandikiza chuki, uhasama, na uharibifu wa Chama miongoni mwa wanaChama na viongozi ameshafanya na kufanikiwa hilo kwa baadhi ya wanaChama na viongozi wake na kuharibu taswira ya Chama kwa jamii. Tunapenda kuwajulisha kuwa suala hili haliwezi kamwe kufananishwa na mgogoro wa kisiasa kati ya CUF na CCM kule Zanzibar, kila mmoja ndani ya CUF amejitoa muhanga kutetea ukombozi wa nchi kwa namna yake wapo waliopigwa, kufungwa jela, kuteswa, kubakwa, kujeruhiwa, waliokimbia nchi, nakadhalika, lakini kubwa zaidi wapo waliopo makaburini hivi sasa kutokana na utetezi kwa Chama chetu cha CUF, wameuwawa na vyombo vya dola. Katibu Mkuu wetu Maalim Seif Sharif Hamad amewekwa ndani (detention) bila kesi miaka mitatu, wengine walisingiziwa kesi za uhaini waliwekwa ndani miaka minne bila ya kesi. Na wengi ya hao ni WanaCUF wa upande wa Zanzibar ambao leo vijana wa Lipumba wanatoa lugha za kejeli dhidi yao.

Mwisho:

WanaChama wa CUF, viongozi wa CUF na watanzania waliowengi wanaamini kuwa Lipumba wa mwaka 2017 siyo Lipumba wa mwaka 2010 kurudi nyuma. Dhamira na malengo yake yamebadilika na hakuna namna ya kukubalika tena kuendelea kuwa kiongozi wa Chama cha CUF. Vyovyote itakavyokuwa kama mshirika wenu wa karibu Jaji Francis Mutungi amewaambia atafuta Chama, CUF na viongozi wake wako tayari kwa lolote na kamwe hawatakubali kuchezewa na kuporwa mamalaka waliyonayo ya kikatiba. Msajili wa vyama vya siasa hana mamlaka na hapaswi kuingilia utendaji wa shughuli za ndani ya chama na kubatilisha maamuzi ya vikao halali vya Chama. CUF na viongozi wake siyo watu wa mchezo mchezo, afanye atakavyo. Lipumba awaombe radhi watanzania na wanaChama wa CUF kwa usaliti na kukubali kutumika kirahisi na kwa thamani ndogo na serikali ya CCM ambayo hapo awali aliipinga kwa nguvu kubwa. Kwa kuwa alikuwa Ngangari. Leo anashindwa kuikosoa hadhani, hakuna uchambuzi wa kiuchumi (Critical thinking) kama alivyokuwa akifanya hapo awali. Leo ni mualikwa wa kila shughuli ya serikali hata pale yanaposemwa maneno yanayokiuka katiba ya nchi anapiga makofi. Lipumba sio mwenzetu tena. Leo ameshindwa kunyoosha maneno, amejikanganya vya kutosha na ameshindwa kujibu maswali aliyoulizwa kwa ufasaha tuliokuwa tunaujua kutoka kwake. Ushauri wetu aende akaendelee na kazi inayohusiana na taaluma yake ya uchumi iwe ndani au nje ya nchi. Kuendelea kuambatana na magenge ya wahuni ambao hawalingani na umri wake na kiwango cha taaluma yake ni kuendelea kujidhalilisha mbele ya jamii. Lipumba ajitafakari upya.

CUF NI TAASISI IMARA YENYE VIONGOZI MAKINI

HAKI SAWA KWA WOTE

____________________________________
MBARALA MAHARAGANDE
K/NAIBU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI
NA MAHUSIANO NA UMMA
MAWASILIANO: 0784 001 408/0715 062 577
MAJIBU YA CUF MAJIBU YA CUF Reviewed by Unknown on 07:54:00 Rating: 5

No comments

Recent